Uncategorized

R.I.P BI KIDUDE

By  | 
Mwanamuziki mkongwe Bi Kidude amefariki dunia leo huko Zanzibar.Bi Kidude amefariki kutokana na maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye kongosho.Mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake mjini Zanzibar.

HISTORIA YA BI KIDUDE KWA UFUPI

Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika.
Jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. (Mwaka aliozaliwa haujulikani
ila anakisiwa kuwa na umri wa miaka 102. amefariki 17 Aprili 2013, Bubu
Zanzibar). Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya
muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
 Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi,
zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. Bi Kidude alikuwa hafahamu
tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alisema kwamba alizaliwa
wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
 HISTORIA HII ILIANDIKWA ENZI ZA UHAI WAKE NA MENGI YAMEKARIRIWA KUTOKA KWAKE.
 Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka
kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi
hizo Sitti binti Saad.
Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika
Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa
wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi
Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia
nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku
nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa
akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.

Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara,
baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha
kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso
aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri
ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling’ara sana katika fani yake ya
uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi
nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.

Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya ‘wanja’ na ‘hina’
ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa
dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa ‘Unyago’ na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.

Watu wanasema ‘Utu uzima dawa’ Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa
akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni
za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani
ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria
tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu.
Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na
kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si
kawaida kwa wanawake Zanzibar.

Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.

Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.

Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang’ombe,ya laiti na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,Amina.
 
Historia hii kwa msaada wa wikipedia.

5 Comments

 1. Anonymous

  April 17, 2013 at 6:04 pm

  Du! Kufa nikwetu wote ila haki zoeleki japo umri aliofikia tuki huzunika sana nikama tuna mkufuru mungu ila tuta mkumbuka kwa mengi liliwemo la kufikisha umri huo r.i.p

 2. Anonymous

  April 18, 2013 at 12:09 pm

  Salam Dinna na ahsante kwa taarifa. Nakusahihisha kidogo japo unasema hii historia kwa msaada wa Wikipedia. Kwanza ni vita ya kwanza ya dunia na si vita ya kwanza ya Ulaya. Pili kuvaa hijabu ni katika mfumo wa kiislam na si kiarabu japo uislam ulianzia huko na kisha kuenea duniani kote. Pia kusema pamoja na kugubikwa na utamaduni wa kiarabu kwamba mwanamke anapotoka hadharani shurti ajifunike, nina hakika haimzuii mwanamke kuwa na upeo mkubwa kwani akili ya mtu haiingiliani na kujifunika ama kutokujifunika na mtu anaangaliwa maneno yake, matendo yake na namna alivyo mweledi na hii haitokani na mavazi. Shukran

  • Anonymous

   April 19, 2013 at 2:00 pm

   swadakta…

 3. Anonymous

  April 19, 2013 at 6:19 am

  inna lillahi wainna ilaihi rajiuna.

 4. ELIUD SAMWEL

  April 21, 2013 at 11:24 pm

  R.I.p bibi yetu

Leave a Reply